Follow CHRIS MAUKI:

www.chrismauki.com

Thank you very much for visiting our blog. We have new website for you,we are sure this new website will completely blow your mind! Subscribe by entering your e-mail below to stay updated on our progress.

Launching
comeback
launchpad

Education & Articles (makala)







ITAMBUE HAIBA YAKO  

 (Know your Personality)




KWANINI UKO VILE ULIVYO?


Vyovyote haiba yako ilivyo na kwa vyovyote unavyowachukulia wale wenye tabia ngumu fahamu kuwa mfano huo ulishakuwepo miaka mingi iliyopita, labda zaidi ukiwa mtoto ndio ilikuwa chanzo cha vile ulivyo leo; Mwanasaikolojia mmoja aliuita mfumo huu “A child is a father of a man” yaani mambo tunayoyaona au unayoyaona kwa mtoto hutupa picha halisi ya ukumbwa wake utakavyokuwa. Zaidi ya asilimia sitini ya yote yanayoendelea maishani mwetu leo yanachangiwa na makuzi yetu tukiwa watoto.


Wengi wetu tumejiharibia misingi yetu ya uwezo wa kuishi na watu wenye tabia ngumu na hivyo kujikuta tunaumizwa tokea tukiwa watoto wadodo. Habari njema ni kwamba hakuna ulazima wa kubaki vile ulivyo, mabadilko yanawezakana, inawekana katika hatua yoyote kubadili mtazamo au muonekano wako na kuboresha ujasiri wako.

Tujaribu kuangalia baadhi ya sababu zinazosababisha mtu kujiona au kujitazama vibaya, hii itakuwezesha wewe kujua uko wapi na kwanini.


  1. Watu wa kwanza kabisa waliowahi kuwa karibu na wewe ni baba na mama yako au yoyote aliyechukua nafasi yao, mfano mlezi, babu, bibi nk. Kutokana na mtazamo wao juu yako, hapo wewe umetengeneza au kuzalisha mtazamo juu yako mwenywe najinsi unavyojithamini au kutojithamini. Kwa lugha rahisi ni kwamba, jinsi unavyojiangalia ulivyo leo kunatokana kwa kiasi kikubwa na jinsi wao walivyokuwa wanakutazama, kama walikuona wewe lofa na mjinga basi kuna uwezekano mkubwa na wewe leo utajiona lofa tu.



Najua wapo wazazi wasio na hekima wala wema kwa watoto wao, huwasababishia watoto wao majeraha ya kimwili, kihisia na hata kiakili, uzuri ni kwamba fungu la wazazi hawa ni dogo. Ingawa inawezekana sana kwa wazazi au walezi au watu wazima wowote kusababisha majeraha na athari kwa watoto mara nyingine pasipo kujua kwamba wanafanya hivyo. Katika kuongea na wazazi lukuki nimegundua kwamba asilimia kubwa ya watoto wameharibiwa na wazazi wao wenyewe, pasipo wazazi hawa kujua kuwa wanawaharibu watoto wao.



  1. Wazazi ambao huwalinda na kuwatetea sana watoto wao, wakijaribu kuwafanyia kila kitu kwa niaba ya watoto hao, kwa njia hii wazazi hawa hutengeneza watu wazima (wababa au wamama) wenye utegemezi mkubwa, wasioweza kufanya kitu chochote wenyewe wala kusimama kwa miguu yao wenyewe. Unakuta hata kazi za shuleni mama ndiyo anafanya, mtoto anakuwa hata kuosha mwili wake hajui, na hawa ndio wale ambao ndoa huwashinda mapemaaa.



  1. Wale wazazi au walezi ambao hutoa mahitaji kwa watoto wao lakini hushindwa kuonyesha kwa matendo upendo wao kwa watoto wao (mfano. Kuongea nao, kucheka nao, kucheza nao n.k.) hutengeneza kizazi kinachoamini kuwa hakipendeki, hakina mvuto, kisicho na thamani na kisichostahili kupendwa. Baba haijalishi unatoa mahitaji yote yanayohitajika nyumbani kwako, hilo sio pekee watoto wako wanalolihitaji kutoka kwako, wape muda wakuwa pamoja nao, waruhuru kucheza na wewe kidogo, toka pamoja nao, jibu baadhi ya maswali yao, waruhusu kujuwa kumbe baba au mama anaweza kuwakaribu na sisi pia.





  1. Wazazi au walezi ambao kila mara humwekea mazingia mtoto kujiona aliyeshindwa, kila wakati ni wakufeli tu, wazazi hawa ni wale wanaosema kwa nini mtoto asijitahidi, kwanini asiwe wa kwanza darasani, ni mpumbavu n.k.. hali hii huharibu kabisa imani ya mtoto kwake yeye mwenyewe, huua kule kujiamini kwake na pia kutokiamini kile anachokifanya.

Yawezekana kuna vitu vilivyoonekana katika makuzi ya mtoto ambavyo hakuna wa kulaumiwa lakini bado vitu hivi huathiri sana kujiamini na kujithamini kwa mtoto yule.

Mtoto au watoto wanaohama hama au kuhamishwa shule mara kwa mara, kwa sababu zao binafsi au kwa sababu ya kuhama hama kwa wazazi hupata shida yakujiona wapweke kwa maana kila wakati hupata kazi ya kutengeneza marafiki wapya na kwamuda fulani hali hii huathiri haiba zao na kujenga kitu tunachokiita “inferiority complex”



Tufanye nini??

Kitu cha kwanza ni kukubaliana na ukweli kwamba mtazamo wako (jinsi unavyojitazama) hubadilika badilika. Tena hubadilika kiasi ambacho mara nyingine huwezi kutambua. Unaweza kuchagua mwenyewe jinsi unavyotaka mtazamo wako uwe. Kwa mfano;


  1. Kufanikiwa au kushindwa

Jaribu kutoangalia nyuma kule ulikowahi kushindwa zaidi, kila mtu anahistoria ya kushindwa sio wewe tu. Wacheza mpira maarufu duniani, mara nyingine hukosa magoli rahisi kabisa lakini hakuna hata mmoja aliye acha kucheza au kuharibu fani yake kwa sababu ya kukosa goli. Wala hakuna aliyekiri kuwa yeye sio bora kwa sababu tu ya kukosa goli moja. Ni vema kukumbuka kule tulikowahi kushindwa kama tu tunataka kujifunza katika makosa yetu, na sio kwa kutaka  kujisononesha na kujilaumu kwa namna tulivyokosea. Jifunze kuziacha historia za kufeli na kushindwa zifukiwe katika yaliyopita.



Tengeneza mafanikio yako wewe mwenyewe anza katika hali ya chini kabisa, chagua vile vitu usivyo viweza kabisa kuvifanya mfano; Kuzungumza mbele ya watu, kuimba, kuogelea, kuwa kwenye usaili, kusimama mbele ya kamera n.k anza kuvifanya kwanza kupitia ufahamu wako (viwaze akilini) hali hii inaitwa (creative visualization) ni njia majawapo bora ya kufanya mazoezi ya vile tunavyoshindwa katika fikra zetu, kwanza jitahidi kujitazama fikrani ukiwa au ukifanya vitu hivyo kwa ushindi hadi ufahamu wako utakapoizoea hali hiyo na kuacha kutuma jumbe za kushtuka (kupanick) au uwoga wakati utakapokuwa unafanya vitu vile kihalisi.



Katika kufanya mazoezi ya kufikiria kimtazamo, chagua kufanya katika utulivu mchana au jioni. Muda kabla hujaenda kulala ni mzuri zaidi. Rudia zoezi hili mara kwa mara mpaka uzoee na fikra zizoee.



  1. Andika vile vitu uvipendavyo juu yako mwenyewe, kama kuna mtu anayesema kuwa hana kitu cha kuandika basi mtuhuyo hajafikiri kwa undani au ni mwongo, kila mtu anakitu chema ndani yake.

Kama ukishaandika vitu hivi, angalia tabia ya vile vitu ulivyoviandika pale, kama vitu hivyo vikifanywa na mtu baki usiyemjua je utasema yeye ni mtu mbaya? Kama sio, kwa nini wewe unajiona usiyefaa na uliyejaa mabaya tu?

Badala ya kutazama yale yaliyo mabaya na yakushindwa katika historia yako tazama mafanikio yako. Kila mmoja ana mafanikio ya aina fulani, hata kama ni madodo kiasi gani. Hata kama unatazama yale yaliyowahi kufanyika huko awali basi yatazame katika mtazamo chanya. 



Wengi wetu hatuchukui muda kujiuliza vyanzo vya mitazamo yetu hasi, tunaamua kuikubali tu na kuikumbatia na kuifanya asili yetu. Ila mara tu utakapo gundua kuwa tatizo sio lako wewe bali ni mazingira uliyokuziwa au aina ya wazazi uliokuwa nao basi utaacha kujidharau.

Wako watoto wanaofurahia kupelekwa shule za bweni mbali na nyumbani, ila wako ambao hawapendi kabisa lakini wanalazimishwa, hali hii hupandikiza ndani ya watoto hawa upweke, hofu, msongo wa mawazo na kutokutulia (nazungumzia utulivu wa ndani) jambo ambalo huendelea hata katika utu uzima wao. Wako wengi ambao tabia zao za leo zilianza kuharibikia katika shule za bweni mbali na wazazi kwa mfano tabia za kusagana au kuingiliana kinyume na maumbile.



Sisi tumeumbwa katika mifumo na vipindi mbalimbali, mara nyingine tuko chanya (watu wema, wazuri) na mara nyingine tunakuwa hasi (watu wabaya). Kama mtoto atakuwa akiambiwa kila wakati kuwa “kamwe huwezi kuwa na akili kama dada yako” maneno haya hufanyika halisi kwake. Je hujawahi kusikia mtu akisema “mimi sijui kuogelea”, “mimi sijui kama nitaolewa” “Kamwe sitokaa niendeshe gari” , “Mimi sitokaa nijue kiingereza”, “Mimi na kuimba ni tofauti” Haimaanishi kama watu hawa wangeanza kujifunza au kuzaliwa katika mazingira ya vitu hivi, wangevishindwa. Labda kuna sehemu mtu au watu fulani waliwasemea kutoweza au kushindwa na huo ukawa mwanzo wa kuwekewa kizingiti cha ujuzi ndani yao.



Wakati wowote mtu anapojisemea jambo, au neno lililo baya, lisilojenga, lakushindwa, kama utalisema kwa sauti au utalifikiria akilini, katika hali yoyote ile jambo hili hulazimisha uhalisi wa maneno yale kuingia katika mfumo wa maisha yako na kutenda kazi kwa hiyo jifunze kukataa, kukanusha na jitahidi kutenda kinyume na zile sentensi mbaya juu yako. Kama tunaamini utendaji wa kazi wa yale tunayojisemea au kusemewa vibaya basi hata yale tunavyojisemea au kusemewa vema hutenda kazi pia. “If negative proclamation works, surely positive proclamation must work too” Amua kubadilisha yale unayojisema au yale unayosemewa. Badili yale yaliyo negative (yakufeli) yawe positive (yakuweza). Kama hujiamini wewe mwenyewe wala hujithamini, basi utakubali kirahisi kila neno gumu na baya utakaloambiwa na kila mwenye tabia ngumu na kama utayakubali unayoambiwa au unayorushiwa hutaweza kamwe kukabiliana na ushindani kutoka kwa mtu au watu wenye tabia ngumu. Kumbuka daima udhaifu huanzia kwako mwenyewe.



Ukishajifunza kupunguza kujilaumu na kujipinga mwenyewe na kuboresha jinsi unavyojitazama basi utakuwa salama katika kukabiliana na maneno na matendo magumu toka kwa yeyote mwenye tabia ngumu. Na kwa kuwa umejifunza vizuri kujielewa basi sasa waweza kuwaelewa vizuri zaidi wale wenye tabia ngumu. Sasa utaweza kuelewa kuwa kuna kitu kimemfanya au kimewafanya wawe vile walivyo. Mara utakapoweza kumwonea huruma yeyote, haijalishi anatisha kiasi gani basi hawezi tena kukuathiri kwa vyovyote vile.



Kwa jinsi ujasiri wako unavyoongezeka, unaweza pia kuziweka katika matendo mbinu nyingine nyingi za kushuhulika na watu wenye tabia ngumu. Utajikuta unaweza kukabiliana nao na pia kuchukuliana nao katika mazingira tofauti na pia hata katika nyakati ambazo hutakuwa unafanya vizuri katika jambo fulani, hautajilaumu na kujishusha, bali utajisifu kwa kukazana na kujitahidi hata kama haukubahatika.

                                    -MWISHO-


Katika utafiti wakuchunguza athari za msongo wa mawazo katika moyo, madaktari Mayer friedman na Ray Roseman waliweza kuwaweka watu katika makundi ya haiba mbili; yaani haiba kundi A and haiba kundi B.


Madaktari hawa waligundua kuwa hata kama kazi na aina ya maisha ingefanana, watu wa haiba kundi A wangekuwa na nafasi mara 3 kuteseka na msongo wa mawazo, magonjwa ya moyo, shinikizo la damu n.k. na watu hawa mara nyingi huwa wanamaudhi kwa jinsi wanavyojibu au kuongea na wengine, na hili limekuwa likiwaongezea msongo wa mawazo maradufu.


Makundi haya yamewekwa ili kukuwezesha wewe kujua uko upande gani. Usichanganyikiwe wala kushtuka pale utakapojikuta una tabia za makundi yote mawili, mara nyingine inaamaanisha kuwa uko vizuri katika kuhakikisha mambo yanafanyika inavyotakiwa au unavyotaka yawe. Ila kama unajikuta unatabia zaidi ya nusu za haiba kundi A inabidi uchukue uamuzi wa kutafuta kubadilika au kubalisha mtazamo ulionao katika maisha, kabla haujajihatarishia maisha yako wewe mwenyewe.

Haiba Aina ‘A’

-     Ni watu wa ushindani katika kila kitu wafanyacho.

-   Watu wenye haiba ya kutumia nguvu na kulazimishisha

-       Hufanya mambo yao mengi kwa haraka

- Huwa na uchu wa kupandishwa vyeo na kujulikana katika jamii. (Hatakama hawana sifa).

- Hutaka sana kujulikana na kuheshimiwa kwa kile walichokifanya.

-  Hukasirishwa kwa haraka na watu au matukio fulani

-   Huongea mara kwa mara kwa kufoka au kwa vitisho

-  Hupenda kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja.

-   Hutembea na hata kula kwa haraka

- Mara nyingi kuchukizwa sana pale wanapocheleweshwa 

-  Hujali sana muda na kukazana kumaliza mambo kwa muda ulipangwa (meating deadlines)

-  Kila mahali huwepo kwa wakati na kwa muda muafaka.

- Mara kwa mara misuli yao ya uso huonyesha, kumaanisha, kuogopesha au ukali.

Haiba Aina ‘B’


-       Sio watu wa ushindani  mfano, makazini, michezoni, masomoni n.k.

-       Ni watu walio rahisi, na huyakubali mazingira, hufanya vitu taratibu na kwa kufuata kanuni.

-       Huendelea na kuchukuliana na hali ya kazi iliyopo.

-       Huridhika na nafasi walinayo katika kijamii.

-       Hawahitaji kujulikana au kutambulika katika jamii au hata katika matukio.

-       Sio rahisi sana kuwaudhi.

-       Mara nyingi hufurahia sana wanapokuwa pekeyao.

-       Ni wavumilivu.

-       Hupendelea kufanyakitu kimoja kwa muda muafaka kabla ya kwenda kwenye kitu kingine.

-       Hutembea, na kula kwa nafasi na utulivu.

-       Hawajali sana na muda, sio wakukimbizana sana na kumaliza kazi.

-       Mara nyingi ni wachelewaji.

-       Nyuso zao ni za kufurahi na sio za mikunjo.

ITAENDELEA WIKI IJAYO. USIKOSE
ALAMA 11 ZA KUKUONYESHA KUWA MPENZI WAKO SIO MWAMINIFU


Kila mmoja atakubaliana na mimi kwamba mahusiano baina ya wapendanao yalikusudiwa kuwa ya upendo, maelewano, kuaminiana, na urafiki wa hali ya juu, kwa bahati mbaya hali halisi siyo hiyo katika mahusiano ya wengi. Wengi wetu wameumizwa kwa mpenzi mmoja au maranyingine wote kutokuwa waaminifu katika mahusiano yao. Kutokuwa mwaminifu hapa namaanisha hali ya mpenzi mmoja kuwa na mahusiano yasiyo rasmi na mpenzi au wapenzi wengine pembeni. Japo jambo hili hufanyika kwa siri sana kwa kuogopa kuharibu mahusiano mtu aliyonayo, wako baadhi ambao wamegundulika na mahusiano yakaathirika kwa kiasi kikubwa na wengine yalikufa kabisa. 


Wako ambao wameweza kuhimili machungu ya kugundua hali ya wapenzi wao kutokuwa waaminifu lakini pia wako ambao imewashinda kabisa kuwa wavumilivu, wako ambao hali hii imewaletea shida kihisia, kisaikolojia na hata kiafya. Kwa bahati mbaya wengi wetu hatuzijui hata dalili au alama zozote zakutujulisha mabadiliko waliyonayo wapenzi wetu ili basi walao tuanze mapema kufanya uchunguzi au kupeana tahadhari kabla makubwa na machungu zaidi hayajatokea. Zifuatazo ni alama zitakazokusaidia kuwa macho mara utakapoona mazingira ya kufanana nazo yanatokea katika mahusiano yenu, alama hizi nimezikusanya katika mazungumzo na baadhi ya watu niliowahi kusaidiana nao kutatua matatizo ya mahusiano yao na pia nikazihakikisha kupitia kusoma vitabu mbalimbali, kwahiyo ninauhakika zitakusaidia kuona uhalisi wa mambo, na yamkini utaona baadhi ya alama ambazo umeshawahi kuzihisi au kuzishuhudia katika mahusiano yako.



  1. Kuongezeka kwa ghafla kwa hali ya kujipenda 



Yawezekana mpenzi wako alikuwa amezoea kuvaa kawaida, hapa simaanishi kutopendeza, na wewe ulikuwa umemzoea katika halifulani ya mavazi au mitindo mara ghafla anabadilika nakuwa mtanashati zaidi, ana badilisha mavazi, anapenda mavazi ya garama, labda alikuwa hatumii manukato lakini gafla anaanza kupenda manukato tena ya garama, anakuwa mtu wakujijali zaidi ya kawaida yake kiasi ambacho hukumzoea. Katika hali hii jaribu kuwa macho zaidi kufahamu nini kilicho sababisha mabadiliko ya gafla kiasi hicho.


2. Kuanza kuchelewa kutoka kazini mara kwa mara 



Sio kwamba kila mtu anapochelewa kutoka kazini basi anakuwa sio mwaminifu, lakini zaidi ya asilimia 75 (kutoka kwente tafiti) ya ambao wamekuwa na mahusiano nje wamekuwa wakitoa visingizio vinavyohusiana na kazi, vikao, mikutano na safari za kikazi, yamkini wewe ni shahidi wa hili. Unaweza kukuta mtu alikuwa anafanya kazi hiyo muda mrefu tu tangia muanze mapenzi yenu, mara gafla hali inabadilika, sikuhizi anachelewa sana kurudi nyumbani, na anaporudi unaweza kutegemea utamwona amechoka kimwili na hata kiakili kwa majukumu ya kazi kuhusiana na asili ya kazi anayoifanya lakini unakuta mtu wala haonyeshi kuchoka, anafuraha kama kawaida. Hali hii inapojitokeza mara kwa mara usichelewe kufungua macho na kudadisi mazingira maana yamkini ni kweli amepata kazi ya ziada ila siyo ile ya ajira unayoijua wewe.


  3. Kupenda kutembea na mipira ya kinga "condoms" mara     kwa mara 
 
Inashangaza maranyingine kusikia mpenzi mmoja anatabia ya kubeba kondom kwenye pochi yake au mfukoni kwa kisingizio kuwa anajali, cha kushangaza zaidi unakuta yuko katika mahusiano na mkewe au mumewe. Yamkini nikweli kunakujali na labda katika mahusiano yenu hili sio la kushtua kwasababu mnajali afya zenu au mnatumia kondomu kwa sababu zaidi ya moja, lakini inakuwaje pale unapogundua kuwa ile kondom uliyokuwa unaiona haipo tena na yamkini wewe hukuhusika katika kuitumia.

4. Mazingira tatanishi ya simu 

 Inawezekana mpenzi wako sio mtu wa kupokea simu au kupiga simu sana, na hivi ndiyo ulivyomzoea, mara gafla simu zinaanza kumiminika mpaka mida ya usiku. Yamkini pia alikuwa yuko huru hata simu yake inapolia waweza ichukua na kumpatia lakini gafla anakuwa na hofu kubwa na kuificha simu yake, nimeongea na wengine ambao wanakwenda na simu hadi bafuni isije ikasikika. Wengine wameanza kuondoa milio katika simu zao wakati haikuwa kawaida yao, wengine wamegundua kila mbinu ya kuweka namba ya siri (password) ngumu hadi mwenyewe anashindwa kuikumbuka wakati mwingine, wako ambao simu zao zikipigwa hawawezi kupokea na kuongea kwa uhuru kama kawaida, ataondoka na kujitenga pembeni akijifanya anaongea kiuaminifu kabisa lakini mtu uliyempenda na umkamzoea unaweza kugundua uhalisi wa anachokiongea kwenye simu na jinsia ya anayeongea naye kwa kumuangalia usoni tu. Yamkini mpenzi wako amepigiwa simu na kwasababu hakuwepo karibu ukaipokea, na mara mpigaji wa simu anapogundua aliyepokea sio mwenye simu anakata simu hiyo gafla, au gafla unagundua kila simu inayopigwa kwenye simu ya mpenzi wako haionyeshi namba au haionyeshi jina. Mazingira kama haya yanapozidi basi jaribu kuchukuwa hatua, yawezekana kuna mvamizi tayari katika mahusiano yenu.

   5.   Harufu ambazo hujazizoea 

Kwa kuwa wapendanao huwa wamezoeana,maranyingi hata aina ya manukato mmoja anayotumia yanakuwa yanajulikana kwa mwenzake, hata kama mmoja hajui jina la manukato  anayotumia mpenzi wake lakini basi atajua walau jinsi yanavyonukia. Sasa hembu fikiri unamkuta mpenzi wako ametokea na anaharufu ya tofauti kabisa na uliyoizoea, yamkini umeisikia harufu hiyo akiwa amerudi toka kazini wakati asubuhi alipoondoka alikuwa na harufu ile uliyoizoea. Najua hali hii inaweza kuwa na sababu zinazoeleweka lakini maranyingine ni ishara ya kuashiria kutokuwepo na uaminifu baina ya mpenzi mmoja. Maranyingine sio harufu bali michubuko katika maeneo fulani ya mwili ambayo hayana maelezo fasaha yalikotokea, iko michubuko mingine ambayo inajieleza na kutia shaka zaidi, yawezekana, ni mpenzi wa kiume lakini unamkuta na ishara za rangi ya midomo (lip sick) kwenye nguo au mwilini, sidhani kama na hapa bado maelezo yake yataingia akilini kiurahisi.

    6.  Tabia za kuanza kukufuatilia sana au kukuganda 

Nimeshawahi kuwa na mazungumzo na watu wajinsia ya kike waliokuwa kwenye mahusiano ambapo wanaume wao walikuwa hawawaachi, watawapeleka kila wanakotaka, nakutoruhusu mazingira ya wapenzi hawa wakike kuwa huru kufanya mambo yao wenyewe, wengine waliitafsiri hali hii kama penzi kubwa sana, yuko aliyeniambia “mpenzi wangu ananipenda sana, yani hawezi niacha mwenyewe, kila sehemu anataka niende nae” baada ya muda mtu huyu aligundua kuwa ile ilikuwa ni ujanja wa kuficha uhalisi wake na kuzuia mazingira ya mpenzi wake wa kike kugundua au kupewa taarifa za tabia zake, na kwa muda mrefu hakugundua mpaka siku alipo pata tarifa za ukweli na ukawa mwisho wa mahusiano yao, tena mwisho wenye uchungu sana. Kuwa macho sana na tabia za mpenzi wako kukuchunguza sana unapotoka, ulipokuwa, ulikuwa nanani, mlifanya nini, nani mwingine alikuwepo, unaenda wapi, kwa muda gani. Yawezekana yote hii ni hali ya kujilinda au kujihisi mdhambi (guilty conscious) inayomsumbua.

    7.  Mabadiliko katika tendo la ndoa "sex" 

Jambo hili laweza kujidhihirisha katika picha mbili tofauti. Kwa kawaida wapenzi huwa na mazoea fulani katika tendo la ndoa, kwa muda waliokaa pamoja kila mmoja humfahamu mwenzake kwa kiasi fulani. Inawezekana likawa jambo la kushangaza pale ambapo gafla unamuona mpenzi wako anapoteza kabisa hamu ya tendo la ndoa, au hata mnapokuwa katika tendo hilo humuoni akifurahia bali anakuwa kama anayelazimishwa au kutohamasishwa na chochote. Kwa upande mwingine unaweza ukakuta mpenzi wako anakuja na ujuzi wa gafla katika mahusiano yenu ya tendo landoa, hali yake ya kukutamani inazidi gafla, anahitaji mapenzi mara kwa mara na hata mnapokuwa katika tendo hilo anadhihirisha utaalamu wa tofauti na ule uliouzoea. Hali hizi mbili zifanyike tahadhari katika kukusaidia kuyatazama mahusiano yenu.

     8. Marafiki wa mpenzi wako kukukwepa 
 

Ni hali yakawaida kuwa karibu au kuzoeana na marafiki wa mpenzi wako, maranyingine mtawasiliana nao kutaka kujua aliko mpenzi wako au kinachoendelea kwao. Inabidi ujiulize sana pale inapotokea gafla wale marafiki wa mpenzi wako uliowazoea, uliokuwa unawapigia simu wakati wowote leo wana kukwepa, na hata simu hawapokei na maranyingine wakipokea hawakupi taarifa yakueleweka au wanakudanganya. Hii yote inawezekana wanamlinda rafikiyao, au wanakosa cha kujibu maana wanajua uhalisia wa kinachoendelea.



  

  9. Kuzungumza sentensi za kutatanisha


Kama nilivyosema awali, wapenzi wengi hujuana kwa mengi, ikiwemo pia namna ya kuzungumza au kuonyesha hisia. Unaweza kukuta katika mapenzi yenu mpenzi wako anaanza kuwa na sentensi ngumu na zisizo kuwa na msingi kwa mfano anasema “kwa jinsi hii sidhani kama tutafika” “mi siamini kama mapenzi yanadumu” “yani ndio maana watu wanashindwa kukaa na mpenzi mmoja” na maranyingine anaweza kukuuliza baadhi ya maswali moja kwa moja ili kukuona utajibuje. Sentensi hizi zina chanzo moyoni, kuwa macho.



    10. Kuzidi kwa tabia za kutoonekana au kuponyoka


Yawezekana mpenzi wako alikuwa na tabia ya kuwepo nyumbani mida isiyokuwa ya kazini au wikiendi, muda mwingi alipenda kuwa na wewe na akiaga basi atasema anakwenda wapi na akimaliza hurudi mapema kwa sababu anakiu ya kuwa nawewe, mara gafla sikuhizi haagi anakwenda wapi, ukiuliza inawezakuwa vita. Anakuwa na vijisafari vingi na vijisababu visivyoisha vya kumuwezesha kuponyoka. Sehemu ya kwenda na kurudi lisaa limoja anaweza kuchukua nusu siku, kila ukiuliza atakwambia nakuja, niko njiani, kuna foleni, nimekwama, na sababu nyingine nyingi sana. Ukiona haya yanazidi ujue kuna la zaidi ya foleni, na hizo sababu zote zinazotolewa zinafunika jambo.



11. Tabia ya kuficha fedha



Ninafahamu fika kwamba suala la uwazi katika mambo yanayohusiana na fedha na matumizi ni tatizo kubwa kwa wapenzi wengi, wengi wamegombana na hata kuachana kuhusiana na jambo hili. Japokuwa hili ni tatizo kwa wengi lakini wako wapenzi ambao wamekuwa na tabia ya kuambiana kwa uwazi matumizi na mapato yao, hakuna kitu wamefanya kuhusu fedha zao pasipo kuambiana na hivi ndivyo mlivyozoeshana, mara ghafla mmoja anaanza kuwa na siri kuhusu fedha zake au matumizi yake, na wala hapendi kuulizwa ulizwa kuhusu suala hilo. Tabia hii ikidhihirika katika mapenzi yenu usichelewe kuchunguza maana kwa kukaa kimya unaweza kujikuta umechelea mwana na maji ya moto.

Na: Chris Mauki: chrismauki57@gmail.com
 




No 8. MAMBO MACHACHE YA KUWASAIDIA WAZAZI/WALEZI
(TIPS FOR PARENTS AND GUARDIANS)
Inawezekana sana ukaishi na watoto au mtoto wako nyumbani lakini akahisi kama vile haupo. Labda kwa lugha nyingine naweza kusema unaweza kuwepo nyumbani kimwili “physically” lakini usiwepo kihisia na kijamii “absent socially and emotionally” na hapa ndipo wazazi na walezi wengi tulipo pasipo kujua na huku tukidhani kuwa mambo yote baina yetu na watoto wetu yako sawa, ukweli ni kwamba hali sio shwari hata kidogo na kwa bahati mbaya mbegu hii mbovu inayopandwa wakati huu inaota na kumea na kuleta uharibifu wa kudumu katika maisha yote ya mwanao au wanao. Nakushauri ujifunze kubadilika.

Hapa nina vitu vichache ambavyo ni mifano tu ya jinsi au namna ya kukuza na kuendeleza ukaribu au uhusiano baina ya wewe mzazi na mtoto wako. Nina watoto wawili wakike lakini nyumbani kwangu huwa kuna watoto zaidi ya wawili mara nyingi. Hii ni kwasababu watoto hawa toka nyumba za jirani wamejenga uhusiano mzuri wa mzazi na mtoto “parent-child relationship” na mimi kuliko walivyo jenga na wazazi wao, kwahiyo kwao kukaa nyumbani kwangu, wakila, kunywa na kufurahia urafiki na hali ya wao kuwa katika “familia” kunawafanya washinde kwengine mchana na wakalale kwingine usiku. Unaweza kutengeza mazingira ya wanao kuwa na mahusiano bora baina ya mzazi na mtoto. Vitu vichache cha kuzingatia

1. Waonyeshe na kuwahakikishia upendo wa kweli. Wasaidie kupunguza au kuondoa hofu wanapokuwa na wewe au kuongea na wewe, watoto wako wanatakiwa wakuheshimu kwa upendo sio kukuogopa.


2. Furaha na upendo wako kwao uwe wa wakati wote, usiwe wa msimu au baadhi ya vipindi. Ukaribu baina yako na wao uwe wa asubuhi ukitoka kwenda kazini au wao wakitoka kwenda shule na hata wanapoimaliza siku yao wakienda kitandani. Ruhusu wakuone na kuhisi uwepo na upendo wako katika ndoto zao. Hii ni pamoja na kuongea nao matarajio yao maishani pamoja na kusoma nao hadithi wakiwa kitandani “bed time stories”.

Bed time stories na Ronel

 Bed time stories na Rommy

 3. Ninapozungumzia kuwa nao kihisia na kijamii “socially and emotionaly” ninamaanisha kuwaruhusu kukugusa, kucheza na wewe, wao kufahamu hisia zako na wewe kufahamu hisia zao. Wakati wote ukiwa nao wahisi mguso wa kihisia wa kipekee kabisa tofauti na wanapokuwa na mwalimu wao au mtu mwingine hapo nyumbani “there must be an emotional connection between you and them”



 Bonding between Ronel and Dad is in progress

4. Wakati unawahimiza kuhusu maisha yao ya baadae na umuhimu wa kusoma na kujifunza ili kuwa na kesho njema hakikisha hauongei maneno tu bali unakuwa nao katika mchakato, waruhusu kukuuliza swali pale wanapohitaji msaada, pata muda hata kama ni mara chache kukaa nao na kushika vitabu vyao vya shule na kuwaelekeza au kusoma nao. Waruhusu wafuate nyayo zako kwa vitendo sio kwa maneno “Be their model”


5. Pamoja na kwamba kuna usafiri wa shule unaowachukua wanao au mwanao kumpeleka na kumrudisha kutoka shule, mara moja moja pata nafasi ya kumwambia “nitakupeleka/tutakupeleka wenyewe leo, au nitakuchukua mwenyewe. Ukipata nafasi hii, ongea naye au nao mambo mbali mbali ya shule, walimu wake, marafiki zake, umuhumu wa kuwa na marafiki wazuri n.k. Unaweza kujifunza mengi sana kutoka kwa mwanao mnapokuwa wenyewe kwenye gari kwa umbali wa kutoka nyumbani wkako hadi shuleni, vitu ambavyo ungekaa miaka hujavigundua kwa kutoka asubuhi na kurudi majogoo.


 Daddy dropping Ronel at school
6. Mara wanapoona wanauhakika wa maisha, furaha na ulinzi ni rahisi kuyaweka mawazo yao katika yale wanayotamani kuyafanya ikiwemo kazi zao za shule na hivyo kufanya vema darasani na maishani kwa ujumla


Ronel is busy at school

Ni ukweli usiopingika kwamba hata kama unatamani vipi kuwa na ukaribu sana na wanao, pale wanapokuwa wengi ki idadi katika familia mchakato huu huathirika na hivyo athari nyingi kuwa hasi “more of negative effect”.

Tuwaruhusu watoto wetu kufurahia uwepo wetu tukiwa hai, ndiyo zawadi pekee kuliko pesa, nyumba, mashamba na magari tunayoweza kuwaachia tukifariki. Let’s have a positive legacy: Your child, your legacy.

Chris Mauki
Social, relationship and counseling psychologist
University of Pretoria
University of Dar es Salaam
chrismauki57@gmail.com


No 7. KATIKA MAHUSIANO

Mara nyingi kwenye mahusiano utagundua kwamba hauhitaji kusema maneno mengi sana kwasababu tija yake inakuwa ndogo sana, badala yake punguza nguvu yako unayoiweka kinywani kwenye kuongea na uruhusu matendo “actions” yathibitishe uhalisia wa kile unachokiongea. Itakufaidia nini au kuleta mabadiliko gani kwenye mahusiano yako kama kila siku unaongea tu pasipo uthibitisho dhahiri wa unachokiongea? “Words are never tangible, actions may do” Kumbuka “actions speaks lauder than words” and it is always better to walk the talk than talking the walk. Nishati yako ya kinywani inayopotea bure ihamishie kwenye akili na mikono yako. Do something that people can see – Chris Mauki

No 6. NI MTAZAMO TU KUHUSU PESA
Pesa, fedha au hela ni kati ya kitu cha ajabu sana ulimwenguni kinachoweza kusababisha furaha na wakati huo huo kusababisha huzuni, aliyenayo anajisikia furaha wakati asiye nayo anajisikia huzuni, pesa hii pia hubadilika badilika majina yake na sifa zake kutokana na mazingira au kazi inayofanya, kwamfano pesa hii ikiwa inalipwa serikalini inaitwa kodi “tax”, ila ikiwa inalipwa kwa mwenye nyumba inaitwa kodi ya nyumba “rent”. Pesa hii hii ikilipwa shuleni au chuoni inabadili jina inaitwa ada, wakati ikipelekwa kanisani kutolewa kama kawaida inaitwa sadaka na kama inatolewa kama sehemu ya kumi ya hela nyingine uliyoipata inaitwa fungu la kumi au “tenth”. Pesa hii pia akipelekewa baba mkwe kwa makusudio ya kumposa mtoto wake itaitwa mahari, wakati ikifika kwenye msiba inabadili jina na kuitwa rambi rambi. Mtoto akipewa na mzazi wake pesa itaitwa fedha ya mfukoni “pocket money” wakati mzazi wa mtoto huyu anapopewa pesa hii na mwajiri inatambulika kama mshahara. Mwanaume akimpa mpenzi wake noti hii hii ataonekana kuwa anajali, lakini akimpa mwanamke mwingine kwa nia ya kuhitaji mapenzi hataonekana kuwa anajali tena bali anahonga na mbaya zaidi huyu anayepokea pesa hii katika hatua hii haitwi tena ampenzi bali malaya. Ikiwekwa sehemu hela hii, mtu akichukua pasipo wengine kujua anaitwa mwizi, na kama aliyeichukua ni mtoto mdogo na ndio anaanza tabia ya kuchukua mara moja moja yeye wanamwita mdokozi, akizoea udokozi huu ndiyo watamwita mwizi, lakini endapo hela hii inachukuliwa kwa nguvu na mabavu, anayeishukua haitwi tena mdokozi wala mwizi bali anaitwa jambazi. Yani hii hela hii ni au ibadili jina lake kutokana na mazingira inavyotumika au ikubadili jina lako wewe kwa jinsi unavyoitumia. Na huu ni mtazamo tu – Chris Mauki


 No 5.TAFITI KUHUSU MAHUSIANO NA MAPENZI
Tafiti zinaonyesha kwamba wanaume wa makabila, nchi na tamaduni mbalimbali ulimwenguni hufanana katika baadhi ya vitu au maeneo yanayowavutia kwa wanawake. Vitu hivi ni umbo la nane au “hourglass figure”, matiti makubwa, kiuno kidogo, tumbo lililonyooka “flat stomach” na hips zilizojaa – Chris Mauki


NO 4. TOFAUTI ZA KIMTAZAMO BAINA YA MWANAUME NA MWANAMKE 
kutana na mwanamke katika tendo la ndoa malengo na matarajio ya wawili hawa katika tendo hili huwa tofauti kabisa. Wakati mwanamke anasukumwa na tumaini lake kwenye upendo, uaminifu na wote kumaanisha “to be commited” katika penzi hilo hata kabla ya kufanya tendo la ndoa, mwanaume yeye cha kwanza na cha muhimu kuliko vyote ni tendo la ndoa, na kiu yake hii huongoza vyote – Chris Mauki


 No 3. KWA WALE WENYE FAMILIA ZENU
Sikatai kabisa kwamba mara nyingi tunakuwa bize sana kama wazazi, tukijishuhulisha na yale yote ambayo yatazisaidia familia zetu kuiona kesho njema, yamkini baba yuko bize na mama hali kadhalika, muda wakuonana au hata kukaa kuongea na watoto wetu unakuwa kitendawili na bado tunaona “it is ok while it is not”. Nashauri hata kama mmejikuta mko bize kuliko mchwa, ni vema mkajitahidi kuwa na wakati wa kula pamoja kama familia. Nirahisi sana mkawepo pamoja kama familia lakini ukajikuta wewe baba labda hata wewe mama miezi imepita haujawahi kukaa mezani kula na wanao. Wengine watapelekewa chakula chumbani, wengine baba anakula pekeyake kwenye kochi, watoto wako kilomita mbili mbali, wengine watoto wanaanza kula kwanza na wazazi wanafuatia, hali zote hizi hazileti mwanya wa kujenga ukaribu baina ya wazazi na watoto. Ipo siri kubwa sana kwenye kukaa pamoja mkila kama familia, kuna vitu vingi sana unaweza kuvisoma kwa mwanao mkiwa mezani mnakula, viko vijitabia vilivyofichika vinaweza kusomeka mnapokuwa mezani na wanao, waweza pia kugundua hali ya mahusiano baina yao wenyewe unapokuwa pamoja nao mezani. Hivi vyote ni ngumu kudhihirika mkiwa meza za mahotelini na kwenye mitoko siku za sherehe, meza ya chakula ya nyumbani mwako ndio eneo muafaka. Hapa ndipo unaweza kufanya “check in” kwa watoto wako kama nilivyoizungumzia kwenye cd yangu ya “Jinsi ya kumlea na kumkuza mtoto mwenye furaha”. Wazazi wengi hatuwajui watoto wetu ingawa tumewazaa sisi wenyewe kwasababu tunakosa nyakati za maana na za muhimu kama hizi ninazozielezea hapa. Wazazi, jifunzeni kujenga panapostahili kujengwa, ili msije kubomoa pasipostahili kubomolewa – Chris Mauki

No 2. INTIMACY AND CHEMISTRY IS SWEETER THAN SEX (UKARIBU NA MVUTO BAINA YA WAPENZI NI MTAMU KULIKO TENDO LA NDOA)

Nimejifunza kwamba ukaribu “intimacy” na mvuto “chemistry” baina ya wapenzi ni vitu vitamu na vyenye ladha zaidi kwenye mahusiano kuliko tendo la ndoa, hii ni kwasababu wakati tendo la ndoa ni tukio lenye muda maalumu ukaribu na mvuto ni vitu endelevu, vinavyotakiwa kupaliliwa na kumwagiliwa kila muda katika maisha yetu ya mahusiano. Sasa kama wewe au nyie furaha yenu ipo tu mnapokutana kimwili basi nikupe taarifa kwamba mnakosa kitu kikubwa sana, mnakosa sehemu yenye utamu wenyewe wa mahusiano, kwasababu furaha yenu inakosa msingi “base” na hivyo haiwi endelevu, kinyume chake mnajikuta ili kufurahiana lazima mkimbilie kwenye kufanya tendo la ndoa, na mnafanya hadi mnachoka na bado mnahisi “something is still missing somewhere” na mara linapokosekana basi mnabaki kama vitu tu na sio watu. Jifunze kuboresha intimacy na chemistry yenu zaidi, You will always enjoy being together hata pale umbali unapotokea kati yenu – Chris Mauki.


No 1. UHUSIANO KATI YA UBONGO WA MWANAUME NA KIU YA TENDO LA NDOA
 Tafiti zinaonyesha kwamba ubongo wa mwanaume unanafasi ya ukubwa mara mbili na nusu zaidi ilivyotengwa kwa kumwezesha kuwa na msukumo, kiu na hamu yakufanya tendo la ndoa “sex”. Nafasihii ipokatika “hypothalamus”. Hii inawafanya kuwaza zaidi na kwakasi zaidi kuhusu fursa, mbinu na mambo yote yahusuyo tendo la ndoa, iwe usiku au mchana na hii pia humfanya mwanaume kuwa tayari kutumika wakati wowote apatapo fursa ya kufanya tendo la ndoa. Kwa utafiti huu inakuonyesha kwamba ukiona mwanaume wako anakaa muda mrefu hafanyi au hahitaji kufanya tendo la ndoa au labda akisema amechoka jiulize sana, labda ubongo wake ndio unashida, au labda anasehemu nyingine anakomalizi ahaja zake, au “intimacy” baina yenu imeshuka sana kiasi kwamba anaona haimfaidii chochote kufanya tendo hilo na wewe (hii ni hatua mbaya zaidi), au labda anatatizo la kiafya (hapa unatakiwa uchunguzi zaidi)   – Chris Mauki

No comments:

Post a Comment

KWA USHAURI ZAIDI

Email : chrismauki57@gmail.com
Mob No:+255713 407182

Total Pageviews

TANGAZA NASI

TANGAZA NASI
+255718-243339 or +255713-407182 / chrissmauki2014@gmail.com
Powered by Blogger.

JITAMBUE KISAIKOLOJIA

JITAMBUE KISAIKOLOJIA

Popular Posts

About Me

Blog Archive